Advertisement

Bobi Wine Adai Maisha Yake Yako Hatarini; Avaa Koti la Kuzuia Risasi Katika Kampeni za Urais Uganda

Bobi Wine Adai Maisha Yake Yako Hatarini

— Mgombea urais wa Uganda kupitia Chama cha Upinzani cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi Ssentamu—maarufu kama Bobi Wine—amesema kuwa maisha yake yako katika hatari kubwa, jambo lililomlazimu kuanza kuvaa koti la kuzuia risasi wakati wa mikutano yake ya kampeni.

Katika kampeni zake za hivi karibuni, Bobi Wine na timu yake wameendelea kukumbana na mvutano mkali kati yao na vikosi vya usalama. Mashuhuda na wafuasi wameeleza kuwepo kwa matumizi ya risasi, mabomu ya machozi, pamoja na kukamatwa kwa baadhi ya wafuasi wa NUP katika maeneo mbalimbali anapofanya mikutano.

Madai Dhidi ya Vyombo vya Usalama

Bobi Wine ameituhumu serikali na vikosi vya usalama kwa “kuingilia kwa makusudi” shughuli zake za kampeni, ikiwemo kuziba barabara anazotarajia kupita, kusambaratisha mikutano yake bila sababu za msingi na kuwakamata wafuasi wake.

Akizungumzia uamuzi wake wa kuvaa koti la kuzuia risasi, Bobi Wine alisema:
“Unajua hatari tunayokabiliana nayo kutoka kwa vyombo vya usalama. Tumepokea taarifa kuwa ninaweza kulengwa. Ingawa koti hili halinipi usalama kamili, tunajaribu kupunguza hatari kadri tuwezavyo. Kwa jumla tunajua kuwa Mungu ndiye mwenye nguvu zaidi.”

Kauli hiyo imezidisha mjadala kuhusu mazingira ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao, huku wafuasi wake wakieleza hofu juu ya usalama wa mgombea wao.

Majibu ya Polisi

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi nchini Uganda, Abas Byakagaba, amepuuzilia mbali madai hayo na kudai kuwa Bobi Wine na wafuasi wake mara kwa mara wamekuwa wakikiuka miongozo ya kampeni iliyowekwa na mamlaka husika.

“Tuna wajibu wa kuhakikisha utulivu wa umma, jambo ambalo ni muhimu kwa uchaguzi wa amani. Hatutakubali vitendo vya uchochezi, matamshi ya chuki, maandamano haramu na kuwashambulia maafisa wa usalama,” alisema Mkuu huyo.

Vyombo vya usalama vimekuwa vikitoa madai kuwa baadhi ya mikusanyiko ya NUP imekuwa ikifanyika bila kufuata taratibu, jambo ambalo chama hicho kinakikanusha kikisema kuwa hatua hizo ni za makusudi kuwakandamiza kisiasa.

Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2026

Wakati hayo yakijiri, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Uganda unaotarajiwa kufanyika Januari 15, 2026, yanaendelea chini ya usimamizi wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda. Tume hiyo imeeleza kuwa inahitaji haraka Shilingi Bilioni 469.5 za Uganda kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kielektroniki vya utambuzi wa wapiga kura (biometric voter verification systems).

Ufadhili huo unatajwa kuwa muhimu ili kuhakikisha mfumo wa utambuzi wa wapiga kura unafanya kazi ipasavyo na kuepusha changamoto zilizoshuhudiwa katika chaguzi zilizopita.

Advertisement

Leave a Comment